Iringa. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeendelea na jitihada za kusogeza huduma zake kwa waandishi wa habari nchini, safari hii ikifika katika Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (Iringa Press Club – IPC), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha tasnia ya habari na kulinda taaluma ya uandishi wa habari.
Akizungumza wakati wa kikao na waandishi wa habari mkoani
Iringa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB),
Wakili Patrick Kipangula, amesema lengo la ziara hiyo ni kutoa elimu kuhusu
majukumu ya bodi, mchakato wa ithibati pamoja na kusikiliza changamoto
zinazowakabili waandishi wa habari ngazi ya mikoa.
Wakili Kipangula amesema bado kuna changamoto ya uwepo wa
watu wanaojihusisha na shughuli za uandishi wa habari bila kuwa na ithibati
halali, hali inayochafua tasnia na kuhatarisha maadili ya kazi hiyo nyeti.
“Tunawaomba waandishi wa habari kushirikiana na Bodi kwa
kuwafichua watu wanaojitambulisha kama waandishi bila kuwa na ithibati. Hatua
hii ni muhimu katika kulinda taaluma, uadilifu na hadhi ya uandishi wa habari
nchini,” amesema Kipangula.
Amefafanua kuwa ithibati si adhabu bali ni chombo cha
kitaaluma kinacholenga kuhakikisha anayefanya kazi ya uandishi wa habari ana
sifa, maadili na uelewa wa misingi ya taaluma hiyo, sambamba na kuwalinda
waandishi halali dhidi ya manyanyaso au changamoto wanapotekeleza majukumu yao.
Aidha, amewahimiza waandishi wa habari kuzingatia sheria,
kanuni na maadili ya uandishi wa habari, akisisitiza kuwa bodi iko tayari
kushirikiana nao kwa karibu katika kujenga tasnia imara, yenye weledi na
inayoheshimika ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Iringa Press Club (IPC) Frank
Leonard amesema ujio wa Bodi ya Ithibati Iringa ni fursa muhimu kwa waandishi
wa habari wa mkoa huo kupata elimu ya moja kwa moja, kuuliza maswali na kupata
ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu ithibati na haki zao za
kitaaluma.
“Tunaiomba JAB kuendelea kusogeza huduma hizi hadi ngazi za
chini zaidi ili waandishi waliopo wilayani na vijijini nao wanufaike,” amesema.
Waandishi wa habari waliohudhuria kikao hicho wamepongeza
hatua ya bodi kufika mikoani, wakisema itasaidia kupunguza mkanganyiko kuhusu
ithibati, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha mshikamano ndani ya tasnia ya
habari.
JAB imeeleza kuwa itaendelea kufanya ziara katika mikoa
mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari,
kuhamasisha ithibati halali na hatimaye kuinua viwango vya taaluma ya uandishi
wa habari Tanzania.



Comments