Skip to main content

Posts

Showing posts from March 8, 2026

Wanawake Wajasiriamali Mafinga Wanufaika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani

Katika kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Mji wa Mafinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa, wanawake wajasiriamali wa eneo hilo wameeleza kufurahishwa na maadhimisho hayo baada ya kupata fursa ya kuonesha na kuuza bidhaa zao kwa wananchi waliohudhuria. Wajasiriamali hao walisema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kutangaza biashara zao, kupata wateja wapya na kubadilishana uzoefu wa kibiashara, jambo linalochangia kuwawezesha zaidi kiuchumi. Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki ni pamoja na Happy Home Decor na Mwanamke Glow Skincare, ambao walitumia nafasi hiyo kuhamasisha wanawake kujitegemea kiuchumi badala ya kutegemea wanaume kwa kila jambo. Walisema mwanamke anapokuwa na shughuli ya kiuchumi inayomwingizia kipato, huongeza uwezo wa kujitegemea, kuchangia maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.    

Mbunge wa Iringa Mjini Afuturisha Watoto Yatima, Aihimiza Jamii Kuwasaidia Wenye Uhitaji

  Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fabian Ngajilo, amewafuturisha watoto yatima wanaolelewa katika vituo vya Dar-Bilaal na Dar-Fatma vilivyopo Manispaa ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuwasaidia watu wenye uhitaji katika kipindi cha mfungo.   Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mbunge Ngajilo aliitaka jamii kuendeleza utamaduni wa kusaidiana na kuwajali watu wenye mahitaji maalum, hususan watoto yatima, wakati wa vipindi vya ibada kama Ramadan na Kwaresima.   Alisema vipindi hivyo vinafundisha upendo, mshikamano na kuwajali wengine, hivyo ni muhimu kwa jamii kutumia fursa hiyo kusaidia makundi yenye uhitaji ili kuboresha maisha yao.   Aidha, aliwataka wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, taasisi na wananchi kwa ujumla kushiriki katika kutoa misaada kwa vituo vya kulelea watoto yatima na watu wengine wenye uhitaji ili kuwapa faraja na matumaini katika maisha yao.