Iringa. Jamii ya Wahaya
wanaoishi Manispaa ya Iringa imefanya sherehe maalumu ya kuuaga mwaka 2025 na
kuukaribisha mwaka 2026 kwa shamrashamra kubwa, katika hafla iliyopewa jina la “Abanywani”
likimaanisha marafiki.
Sherehe hiyo iliyofanyika
mwishoni mwa wiki jijini Iringa iliwakutanisha Wahaya kutoka maeneo mbalimbali
ya mkoa huo wakiwemo familia, vijana na wazee, kwa lengo la kuimarisha
mshikamano, kuendeleza utamaduni wao na kusherehekea mafanikio ya mwaka uliopita.
Akizungumza wakati wa hafla
hiyo, mmoja wa waandaaji Kaijage Rwezaula alisema neno Abanywani
linaakisi urafiki, upendo na umoja miongoni mwa wanajamii, huku likiwaalika pia
watu wa makabila mengine kushiriki na kujifunza utamaduni wa Kihaya.
“Tumekutana hapa si tu kwa
ajili ya burudani, bali kuimarisha undugu wetu na kusaidiana kama marafiki na
ndugu tunaoishi mbali na nyumbani,” alisema Kaijage
Katika sherehe hiyo,
washiriki walipata fursa ya kufurahia vyakula vya asili ya Kihaya, muziki wa
asili pamoja na burudani mbalimbali zilizochagiza utamaduni wa kabila hilo
linalotoka mkoa wa Kagera Region.
Baadhi ya wazee walitumia
nafasi hiyo kuwakumbusha vijana umuhimu wa kudumisha mila na desturi, huku
wakihimiza mshikamano na maadili mema katika jamii. Pia kulikuwa na sala na dua
za kuombea mwaka mpya wa 2026 uwe wa mafanikio, afya njema na amani.
Washiriki waliozungumza kwa
nyakati tofauti walieleza kufurahishwa na wazo la kuanzisha mkusanyiko huo wa
kila mwaka, wakisema unawasaidia kukutana, kubadilishana mawazo na kujenga
mtandao wa kusaidiana kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa waandaaji,
sherehe ya Abanywani inatarajiwa kuwa tukio la kudumu litakalofanyika
kila mwisho wa mwaka, likiwaunganisha Wahaya na marafiki zao wanaoishi mkoani Iringa
na maeneo ya jirani.
Hafla hiyo ilihitimishwa
kwa nyimbo za pamoja, pongezi na salamu za heri ya mwaka mpya, huku kaulimbiu
kuu ikiwa ni umoja, urafiki na maendeleo kwa wote katika mwaka 2026.
Comments