Mafinga. Baraza la
Madiwani la Halmashauri ya Mji Mafinga limepitisha rasimu ya Mpango na Bajeti
ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya Sh38,651,155,000, katika kikao
kilichofanyika Februari 21, 2026, kikilenga kuimarisha huduma za kijamii na
kuchochea maendeleo ya mji huo.
Akiwasilisha rasimu hiyo kwa
niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Mipango na Uratibu wa Mji, Peter
Ngusa, alisema halmashauri imejipanga kukusanya na kutumia fedha hizo katika
utekelezaji wa majukumu ya msingi, miradi ya maendeleo na kuboresha ustawi wa
wananchi.
Alifafanua kuwa kati ya fedha
hizo, Sh8,844,800,000 zinatarajiwa kukusanywa kutoka mapato ya ndani,
Sh942,454,000 ni ruzuku ya matumizi mengineyo (OC), Sh23,376,336,000 ni ruzuku
ya mishahara, na Sh5,487,565,000 ni ruzuku kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa mpango huo,
vipaumbele vilivyowekwa ni pamoja na kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya
ndani, kununua maeneo kwa ajili ya uwekezaji, kuendeleza shamba la parachichi
la Makalala, kuimarisha miradi ya kimkakati, kuboresha huduma za jamii na
kuimarisha usafi pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu
wa Wilaya ya Mufindi, Linda Selekwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji
Mafinga, Fidelica Myovela, Mwenyekiti wa Halmashauri, Regnant Kivinge,
Mbunge wa Viti Maalum – Vijana kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jasmine
Ng’umbi, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevelle
maarufu kama ‘Villa’.
Mikopo ya Asilimia 10 Yapewa Kipaumbele
Akichangia hoja ya bajeti, Ng’umbi alimuomba Mkurugenzi kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu inatolewa bila urasimu na ucheleweshaji usio wa lazima.
Alisema kumekuwapo malalamiko
kutoka kwa vikundi vinavyoomba mikopo hiyo lakini kucheleweshewa au kunyimwa
bila sababu za msingi, hali inayokwamisha jitihada za kuwawezesha wananchi
kiuchumi.
“Mikopo hii ni haki ya makundi
maalumu kwa mujibu wa sheria na miongozo ya Serikali, hivyo ni muhimu kuweka
utaratibu wazi na wa haki,” alisisitiza Ng’umbi.
Kwa upande wake, Lutevelle
aliwataka vijana wanaofanya shughuli katika Stendi ya Mabasi Mafinga kuimarisha
umoja na kujiunga katika vikundi vinavyotambulika ili waweze kunufaika na
mikopo, mafunzo na mitaji kupitia mipango ya uwezeshaji.
Katika kuonesha dhamira ya kuwaunga mkono, wabunge hao walichangia jumla ya Sh700,000 taslimu kusaidia vikundi vya vijana vinavyofanya shughuli katika eneo hilo.
Changamoto ya Maji Yatajwa
Wakati huohuo, wajumbe wa Baraza
la Madiwani walieleza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama,
wakibainisha kuwa ni asilimia 68 tu ya wakazi wa Mafinga wanaopata huduma hiyo
kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mafinga (MUWASA).
Wameiomba Serikali kuharakisha
utekelezaji wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh48 bilioni unaoendelea, ili
kuongeza wigo wa huduma na kufikia wananchi wengi zaidi.
Baada ya majadiliano ya kina,
Baraza la Madiwani lilipitisha rasmi bajeti hiyo na kuahidi kusimamia kwa
karibu utekelezaji wake ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya kwa wananchi wa
Mafinga.








Comments