Kutokana na matokeo hayo, shule imefanikiwa kushika nafasi ya pili ngazi ya halmashauri, ikiendelea kuonesha mwelekeo chanya wa kitaaluma na ushindani bora miongoni mwa shule za sekondari za manispaa hiyo.
Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Robert Ngimba, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wanafunzi na wazazi, pamoja na kuimarika kwa nidhamu, ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi na utoaji wa masomo ya ziada kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum.
Ameeleza kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 1998 na hadi sasa imekuwa na wakuu wa shule wanne waliomtangulia, yeye akiwa wa tano.
“Shule yetu inaendelea kukua kitaaluma. Mwaka 2024 tulifanikiwa kufaulisha wanafunzi wote na kufuta daraja la sifuri katika mitihani ya taifa ya Kidato cha Nne. Mwaka 2025 pia wanafunzi wote 150 waliofanya mtihani walifaulu, hivyo kuendelea kufuta daraja la sifuri kwa mwaka wa pili mfululizo,” amesema Mwl. Ngimba.
Aidha, shule hiyo imeongeza ufaulu bora (Division I–III) hadi kufikia asilimia 65, hatua inayoonesha kuimarika kwa ubora wa matokeo. Katika ngazi ya halmashauri kwa shule za serikali, Mawelewele imeshika nafasi ya pili ikitanguliwa na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa.
Katika ngazi ya mkoa, kati ya jumla ya shule 154, ni shule 12 pekee zilizopata tuzo ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, na Mawelewele ikiwa miongoni mwa shule hizo 12 bora.
Akizungumzia siri ya mafanikio hayo, Ngimba amesema ni kujituma kwa watumishi, kuwa na lengo la pamoja, usimamizi madhubuti na walimu kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa kwa ubora, sambamba na ushirikiano mzuri kati ya shule, wazazi na wanafunzi.
Ametoa shukrani za pekee kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha za elimu bila malipo, ambazo zimesaidia kutatua changamoto mbalimbali shuleni hapo. Pia, utaratibu wa wanafunzi kupata chakula cha mchana umeongeza muda wa kujisomea na kuimarisha umakini darasani.
Wadau wa elimu wamesema mafanikio hayo ni ishara kuwa mikakati iliyowekwa imeanza kuzaa matunda, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza ari hiyo ili shule iweze kushika nafasi ya juu zaidi katika matokeo yajayo.







Comments