Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika mazishi ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar
es Salaam, Marehemu Polycarp Pengo.
Ibada ya mazishi imefanyika
katika Kanisa la Hija ya Bikira Maria – Pugu, jijini Dar es Salaam, ambapo
waumini na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali walihudhuria kutoa heshima
zao za mwisho.

Akitoa salamu za rambirambi baada
ya ibada, Dkt. Nchimbi amesema Serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa
alioutoa Kardinali Pengo katika maendeleo ya nchi, kiroho na kimwili. Alisema
marehemu alijitoa si kwa Wakatoliki pekee, bali kwa Watanzania wote bila kujali
tofauti za imani.
Ameeleza kuwa Kardinali Pengo
alikuwa kiongozi mwadilifu aliyesisitiza kuishi maisha ya kufuata amri za Mungu
na kuheshimu sheria za nchi. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, maadili
aliyoyafundisha na kuyaishi yanapaswa kuwa mwongozo kwa kila Mtanzania.
Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa
marehemu atakumbukwa kwa juhudi zake katika kukuza maendeleo ya jamii, hususan
katika sekta za elimu, afya, maji na huduma kwa watu wenye mahitaji maalum.
Amesema ni wajibu wa Watanzania kuuenzi mchango wake kwa kuishi kwa uadilifu na
kuzingatia sheria.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi
wa dini kuendelea kuliombea taifa na viongozi wake ili waweze kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi.
Mwili wa Marehemu Kardinali Pengo
umezikwa katika Kituo cha Hija ya Bikira Maria – Pugu, Dar es Salaam, huku
Serikali na Kanisa Katoliki wakimwelezea kama kiongozi aliyeacha alama ya
kudumu katika historia ya nchi.




Comments