Mufindi. MBUNGE wa Jimbo la
Mufindi Kusini, David Kihenzile, amezindua Kituo cha Afya cha Makungu
kilichojengwa kwa gharama ya Sh milioni 500 katika Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi, hatua inayotarajiwa kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma za
afya kwa zaidi ya wananchi 17,000 wa kata hiyo na maeneo ya jirani.
Kukamilika kwa mradi huo
kunatajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan
ndani ya siku 100 za mwanzo wa muhula wake mpya wa uongozi baada ya Uchaguzi
Mkuu, ambapo Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya afya na kusogeza
huduma karibu na wananchi.
Akizungumza leo Februari 23,
2026, wakati wa ziara yake ya siku nne jimboni humo, Mbunge Kihenzile ambaye
pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, alisema ujenzi wa kituo hicho ni mkombozi
mkubwa kwa wakazi wa Makungu, Mgololo na maeneo ya jirani waliokuwa wakilazimika
kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, hususan huduma za mama na mtoto.
Alisema kipindi cha mvua wananchi
wa ukanda wa Mgololo wamekuwa wakikumbana na adha kubwa kutokana na miundombinu
kuwa hafifu, hali iliyosababisha baadhi yao kushindwa kufika hospitali kwa
wakati.
“Kipekee tunamshukuru sana Rais
Dk. Samia Suluhu Hassan. Tulimfikishia ombi maalumu kuwa Makungu ni kata
muhimu, na Mgololo ni ukanda ambao wakati wa mvua wananchi hupata tabu kubwa;
wapo waliokuwa wanapoteza maisha kwa kukosa huduma za afya kwa wakati. Leo
tunajivunia kuwa na kituo cha afya kitakachohudumia Makungu pamoja na maeneo ya
Idete na Kiohela,” alisema Kihenzile.
Wananchi waliohudhuria hafla ya
uzinduzi walieleza kuwa kituo hicho kitapunguza gharama za usafiri, kuokoa muda
na kuongeza upatikanaji wa huduma za dharura, jambo litakalochochea maendeleo
ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.








Comments