Mbarali. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Jamhuri iliyopo Kijiji cha Ilongo, Kata ya Ilongo wilayani Mbarali mkoani Mbeya, wameanza kunufaika na mradi wa maji safi uliotekelezwa na Rufiji Basin Water Board kupitia Mradi wa NBS-USANGU.
Kabla ya utekelezaji wa mradi
huo, wanafunzi walilazimika kutembea zaidi ya kilometa tatu kutafuta maji, hali
iliyokuwa ikiathiri mahudhurio yao, kuongeza uchovu na kuchelewesha masomo.
Wengine walilazimika kufika shuleni wakiwa wamechoka, jambo lililopunguza
umakini darasani.
Kupitia mradi huo, kisima kirefu
kimechimbwa na maji kusambazwa moja kwa moja shuleni pamoja na kwa wananchi wa
maeneo jirani, hatua iliyoboresha mazingira ya kujifunzia na kuimarisha
usalama wa wanafunzi.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi hivi karibuni , Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jenifer Sanga, alisema
upatikanaji wa maji ndani ya shule ni mabadiliko makubwa kwa ustawi wa
wanafunzi.
“Hii ni faraja kubwa kwetu. Sasa
wanafunzi hawatapoteza muda kutafuta maji na wataweza kujikita zaidi katika
masomo yao. Tunaamini hata ufaulu utaongezeka kwa sababu mazingira
yameboreshwa,” alisema Sanga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilongo,
Benjamini Mwakalonge, alisema mradi huo umekuwa suluhisho la changamoto ya muda
mrefu ya maji katika eneo hilo.
“Tunashukuru kwa kuifikia jamii
yetu. Maji haya yatasaidia si wanafunzi tu bali pia wananchi wanaozunguka shule
hii. Sasa tunapata maji karibu na makazi,” alisema Mwakalonge.
Hata hivyo, ushirikiano kati ya
Serikali ya Japan na Tanzania umeendelea kuimarika kupitia miradi ya maendeleo
inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini
yenye changamoto za miundombinu ya maji.
imelezwa kuwa uwekezaji katika
sekta ya maji ni hatua muhimu katika kuboresha afya, elimu na ustawi wa jamii
kwa ujumla, akisisitiza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama ni msingi wa
maendeleo endelevu.
Mradi huo umetkelezwa na Rufiji
Basin Water Board kupitia Mradi wa Kuimarisha Mbinu za Asili za Kijamii za
Usimamizi wa Vyanzo vya Maji na Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (NBS-USANGU),
unaofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia World Bank.
Kupitia mradi huo, wanafunzi wa
Shule ya Msingi Jamhuri sasa wananufaika si tu kwa kupata maji karibu, bali pia
kwa kuimarika kwa mazingira ya usafi shuleni, jambo linalotarajiwa kupunguza
magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza
kwa furaha walisema awali walikuwa wakichelewa kufika shuleni au kushindwa
kuhudhuria vipindi vya asubuhi kwa sababu ya jukumu la kutafuta maji, lakini
sasa wana muda wa kutosha wa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli
za shule.
Uongozi wa shule umeeleza kuwa
uwepo wa maji utasaidia pia kuanzisha bustani za shule na miradi midogo ya
lishe, itakayochangia kuboresha afya za wanafunzi na kuongeza ari ya kujifunza.
Kwa ujumla, mradi huo umeonekana
kuwa kichocheo cha mabadiliko chanya katika Kijiji cha Ilongo, ukionesha namna
usimamizi endelevu wa rasilimali za maji unavyoweza kuleta matokeo ya moja kwa
moja katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.


.jpeg)
.jpeg)
Comments