Idara ya Vijana ya Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Usharika wa Kanisa
Kuu Iringa, kwa kushirikiana na huduma ya The Healing Missionaries kutoka Dar
es Salaam, imeandaa mkesha mkubwa wa kusifu na kuabudu utakaofanyika Machi 20,
2026 mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri
James, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo la kiroho linalolenga
kuwakutanisha waumini na wananchi kwa pamoja katika kumsifu na kumshukuru
Mungu.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Luckson Luswema maarufu kama Kaka MC Mtumishi, amesema lengo la mkesha huo ni kumsifu Mungu na kumshukuru kwa mambo
makuu aliyowatendea, huku akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi
kushiriki ibada hiyo ili kupokea baraka mbalimbali zitakazopatikana.
Aidha, ameeleza kuwa mgeni
mwenyeji atakuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville, ambaye
ataungana na viongozi wengine wa dini kuongoza ibada hiyo maalum.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa The Healing Missionaries, Mchungaji Patrick Mulunda, amesema taasisi hiyo imejikita katika kupeleka habari njema katika maeneo mbalimbali ambayo huduma haijafika, kwa lengo la kueneza Injili na kuwafikia watu wengi zaidi.
Mkesha huo unatarajiwa kupambwa
na waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili, sambamba na ushiriki wa viongozi wa
dini na kijamii, katika tukio hilo maalum lenye lengo la kuimarisha imani,
kukuza umoja na kumtukuza Mungu.




Comments