Tukio hilo lilitokea katika
barabara ya njiapanda ya Tosamaganga–Luhota, wilayani Iringa, ambapo magari
yaliyokuwa yamebeba waombolezaji yalishindwa kupita kutokana na matope na
utelezi mkali.
Waombolezaji hao waliondoka
mjini Iringa majira ya saa 8 mchana, baada ya ibada ya kuaga mwili iliyofanyika
katika Mtaa wa Mwimbi B, Kata ya Makorogoni. Msafara huo ulikuwa ukielekea
kwenye makaburi ya familia ya kina Myulla yaliyopo Luhota, Kata ya Ikuvilo,
wilayani Iringa.
Baadhi ya waombolezaji
walilazimika kushuka kwenye magari na kusukuma ili kujaribu kuvuka eneo hilo,
huku wengine wakilazimika kusubiri kwa muda hadi hali ya barabara iliporuhusu
safari kuendelea.

Wakizungumza kwa masikitiko,
baadhi ya wananchi walisema changamoto ya barabara hiyo imekuwa ya muda mrefu
kila kipindi cha mvua, na kuiomba serikali kuingilia kati ili kuimarisha
miundombinu katika eneo hilo.
Wakati huohuo, wananchi wa
Kijiji cha Ikuvilo, Kata ya Luhota, wameeleza kero ya kukosa zahanati na huduma
ya umeme. Wamesema hali hiyo imekuwa ikiwasababishia usumbufu mkubwa, hususan
wakati wa dharura za kiafya na shughuli za kiuchumi.
Wananchi hao wamepeleka kilio
chao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,
wakimuomba awasaidie kupata huduma za msingi ili kuboresha maisha yao.







Comments