Na Hawa Matias, Mbeya
Mbeya, Machi 07, 2026 – Taasisi
ya Tulia Trust, chini ya uongozi wa Dkt. Tulia Ackson, Rais wa Umoja wa Mabunge
Duniani (IPU) na Mbunge wa Jimbo la Uyole, imemkabidhi nyumba ya kuishi familia
ya Mzee Tuli Mwalwala Mwantindili.
Nyumba hiyo, iliyojengwa kupitia
mpango wa Tulia Trust – Mtaani Kwetu, ni nyumba ya 23 kwa ajili ya watu wenye
uhitaji. Kwa nyumba hizo, nne (4) zimejengwa nje ya Jiji la Mbeya. Familia ya
Mzee Mwantindili inayoishi mtaa wa Itongo, Kata ya Mwakibete, imepata makazi
mapya leo.
Akizungumza katika hafla ya
makabidhiano, Dkt. Tulia aliwaasa wananchi wa kata hiyo kuendeleza utamaduni wa
kusaidiana na kushirikiana katika changamoto mbalimbali zinazowakabili baadhi
ya wananchi.
"Sisi kama jamii tuendelee
kushirikiana na kusaidiana kwenye changamoto mbalimbali tulizonazo hata kwa
kidogo tulichonacho," alisema Dkt. Tulia.
Aidha, Dkt. Tulia ametoa iftari
kwa waumini 1,000 wa dini ya Kiislam katika hafla fupi iliyoandaliwa nyumbani
kwake, Kata ya Utezi, Jijini Mbeya. Hafla hiyo pia ilihusisha viongozi
mbalimbali wa jamii na ni utaratibu wake wa kila mwaka kufanya tukio hili
katika kipindi cha mifungo.


.jpeg)
Comments