Iringa. Marehemu William Lukuvi, aliyewahi kuwa Waziri na Mbunge wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa, anakumbukwa kama kiongozi mwenye moyo wa kujitolea, aliyeacha alama isiyofutika katika maisha ya wananchi na maendeleo ya jamii.
Ndani na nje ya siasa, Lukuvi
alijijengea heshima kutokana na misingi yake ya haki, usawa na upendo kwa watu,
hali iliyomfanya kupendwa na kuaminiwa na makundi mbalimbali ya jamii.
Kwa mujibu wa Thom Lukuvi,
aliyemtaja marehemu kama “baba mdogo,” familia inamkumbuka kama nguzo muhimu
iliyodumisha mshikamano na ustawi wa ukoo. Alisema marehemu hakuwa tu kiongozi
wa kisiasa bali pia mlezi na mshauri aliyekuwa tayari kusaidia mtu yeyote
aliyehitaji msaada.
“Alikuwa mtu wa watu, hakubagua.
Alisikiliza changamoto za kila mmoja na kujitahidi kuzitatua kadri ya uwezo
wake,” alisema Thom.
Aliongeza kuwa pale ambapo hakuwa
na uwezo wa kusaidia, Lukuvi hakutoa ahadi zisizotekelezeka bali alichagua
kusema ukweli, jambo lililoongeza uaminifu wake kwa wananchi.
Familia pia imeeleza kuwa misingi
ya haki na ukweli ndiyo iliyomuongoza katika maamuzi yake, akisimamia usawa
bila upendeleo, hali iliyomfanya kuwa mfano wa kuigwa kwa wengi.
Wakati huo huo, wanafunzi wa
shule ya sekondari iliyopo Pawaga, iliyopewa jina la Lukuvi kufuatia mchango
wake katika ujenzi wake, wamemkumbuka kwa matendo yake ya ukarimu na kujali
elimu.
Mmoja wa wanafunzi hao, Natasha
Simbaya, alisema marehemu aliwahi kuwatembelea shuleni na kuwapatia chakula
pamoja na vinywaji wakati wa sikukuu ya Idd, jambo lililowaacha na kumbukumbu
isiyosahaulika.
“Alituletea mchele na soda,
tukapika pilau na wali. Ilikuwa furaha kubwa kwetu,” alisema Natasha.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu
wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga, amemuelezea Lukuvi kama kiongozi aliyetoa
mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta za elimu, afya na ajira.
Alisema Lukuvi alisimamia ujenzi
wa shule nyingi na kuanzishwa kwa taasisi za mafunzo ya ufundi stadi (VETA),
hatua iliyosaidia kuongeza fursa kwa vijana kujiajiri.
Aidha, alibainisha kuwa marehemu
alikuwa mstari wa mbele kusukuma ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Iringa katika
kijiji cha Igodikafu, hatua iliyopunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu
kufuata huduma za afya.
“Alikuwa kiongozi wa vitendo
aliyesikiliza wananchi na kuchukua hatua. Mchango wake utaendelea kukumbukwa
vizazi na vizazi,” alisema Kiswaga.
Wananchi wa Isimani na Mkoa wa
Iringa kwa ujumla wameeleza masikitiko yao kufuatia kifo cha kiongozi huyo,
wakimtaja kama nguzo muhimu ya maendeleo aliyeacha pengo kubwa.
Mazishi ya marehemu yanatarajiwa
kufanyika kwa heshima zote stahiki, huku viongozi mbalimbali wa Serikali na
wananchi wakitarajiwa kushiriki kumuaga kiongozi huyo aliyegusa maisha ya
wengi.


Comments