MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imemhukumu kunyongwa hadi kufa,
Joseph Muhulila (28), mkazi wa Mtaa wa Lukosi, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya
Iringa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi mtoto wake wa
kumzaa, Timothy Muhulila (miaka 4), akidaiwa kufanya hivyo kwa imani za
kujipatia utajiri.
Hukumu hiyo iliyosomwa kwa zaidi ya saa nne imetolewa na
Jaji Angaza Mwipopo katika kesi namba 25532 ya mwaka 2025, akieleza kuwa
ushahidi uliowasilishwa mahakamani umethibitisha bila kuacha shaka kuwa
mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya
Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka 2022.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili David Mwakiborwa
na Jackson Mwakalinga.
Kwa mujibu wa mahakama, tukio hilo la kikatili lilitokea
Aprili 12, 2025, ambapo mshtakiwa alimuua mtoto wake kisha kumkatakata vipande
vidogo na kuvitupa kwenye shimo la choo.
Akisoma maelezo ya ushahidi, Jaji Mwipopo alinukuliwa
akisema:
“Mtuhumiwa alikiri kukata mwili wa marehemu vipande vidogo
na kuviponda mifupa kwa jiwe kubwa kabla ya kuvitupa kwenye shimo la choo.”
Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa, mabaki ya mwili
yalipatikana katika tenki la maji taka na kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu wa
vinasaba (DNA), ambapo majibu yalionesha kwa asilimia 99 kuwa yalihusiana na
marehemu.
Mahakama ilieleza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha
mashahidi 13, ambao ushahidi wao uliisaidia kufikia uamuzi wa kumtia hatiani
mshtakiwa na hatimaye kumhukumu adhabu ya kifo.
Hata hivyo, wakili wa utetezi, Geoffrey Mwakasege, amepinga
hukumu hiyo akidai kuwa mahakama haikuzingatia ipasavyo vielelezo muhimu
vilivyowasilishwa.
Alivitaja vielelezo hivyo kuwa ni pamoja na ramani ya eneo
la tukio, ripoti ya uchunguzi wa DNA pamoja na maelezo ya onyo ya mshtakiwa.
Mwakasege alidai kuwa kulikuwa na mkanganyiko katika
ushahidi wa kitaalamu, akieleza kuwa mtaalamu wa DNA alidai kupokea vipande vya
mifupa pekee, huku baadhi ya mashahidi wakidai waliona vipande vya nyama, jambo
lililoleta sintofahamu.
Aidha, alieleza kuwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa hayakuwa
na saini yake, hali iliyosababisha mahakama kutoyazingatia.
Aliongeza kuwa mahakama iliegemea zaidi katika hoja kwamba
mtoto alipotea akiwa mikononi mwa mshtakiwa, jambo lililochangia kwa kiasi
kikubwa hukumu hiyo.
“Mahakama yenyewe imekiri kuwepo kwa mashaka katika ushahidi
wa DNA, lakini bado imetoa adhabu hiyo licha ya uwepo wa walakini,” alisema
Mwakasege.
Pia alidai kuwa ushahidi uliopatikana katika shimo la choo
haukuweza kuthibitishwa moja kwa moja kuwa ni wa viungo vya binadamu, jambo
linaloacha maswali kuhusu msingi wa hukumu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, wakili huyo alisema upande wa utetezi
haujaridhishwa na uamuzi wa mahakama, na kwamba mshtakiwa ana haki ya kukata
rufaa iwapo ataona inafaa.
Kesi hiyo imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi
kutokana na ukatili wa tukio hilo, huku wengi wakitoa wito kwa jamii kuachana
na imani za kishirikina na kujiepusha na vitendo vya kujipatia mali kwa njia
zisizo halali.



Comments