Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, leo Ijumaa Machi 6, 2026 amewataka wafanyabiashara kufanya biashara katika maeneo rasmi waliyopangiwa ili kusaidia kuweka miji katika mpangilio mzuri na kuepusha msongamano usio wa lazima.
RC James alitoa kauli hiyo wakati
akifunga kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika mkoani
Iringa. Katika kikao hicho pia alipangua hoja ya baadhi ya wajumbe
waliopendekeza Iringa kupandishwa hadhi na kuwa jiji, akisema bado kuna masuala
ya msingi yanayohitaji kufanyiwa kazi kabla ya kufikia hatua hiyo.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea
kuboresha miundombinu, mipango miji na huduma za kijamii ili kuhakikisha mkoa
unakuwa katika mpangilio unaokidhi vigezo vya kuwa jiji.
Wakati huo huo, Mbunge wa Kilolo Ritta
Kabati pamoja na Mbunge wa Iringa Mjini Fadhili Ngajilo walitoa mapendekezo
mbalimbali kuhusu namna ya kuwasaidia wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama
machinga kufanya biashara zao katika mazingira bora bila kuathiri mpangilio wa
miji.
Wabunge hao walisisitiza umuhimu
wa kutenga na kuandaa maeneo maalumu kwa ajili ya machinga ili waweze kufanya
biashara zao kwa utaratibu huku wakichangia katika kukuza uchumi wa maeneo yao.




Comments