Daktari wa Mifugo Mfawidhi wa ZVC Iringa, Dkt. Jeremia Choga
(L) wakati wa zoezi la uchukuaji sampuli.
Na Friday Simbaya, Iringa
Ugonjwa wa Mapele Ngozi (Lumpy Skin Disease - LSD)
umeendelea kuwa miongoni mwa magonjwa hatari yanayoathiri mifugo, hususan
ng’ombe, na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji kutokana na gharama za
matibabu na vifo vya wanyama.
Hivi karibuni, ugonjwa huo umeripotiwa kushambulia maeneo ya
Nyanda za Juu Kusini, hasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe,
hali iliyosababisha taharuki kwa wafugaji. Takwimu zinaonesha kuwa takribani
ng’ombe 750 wameathirika na baadhi kufa katika kipindi cha Februari hadi Machi,
2026 wilayani humo.
Kufuatia mlipuko huo, Serikali kupitia wataalamu kutoka
Kituo cha Huduma za Mifugo Nyanda za Juu Kusini (ZVC Iringa) na Taasisi ya
Chanjo za Mifugo Tanzania (TVI), wameweka kambi wilayani Momba kwa ajili ya
kufuatilia hali ya ugonjwa huo na kuchukua sampuli kutoka kwa wanyama
walioathirika.
Lengo la zoezi hilo ni kufanya uchunguzi wa kisayansi
maabara utakaosaidia kubaini chanzo cha ugonjwa na hatimaye kuzalisha chanjo ya
kudhibiti na kuzuia maambukizi yake.
Akizungumza wakati wa zoezi la uchukuaji sampuli, Daktari wa Mifugo Mfawidhi wa ZVC Iringa, Dkt. Jeremia Choga, alisema serikali inaendelea kuwajali wafugaji kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za mifugo ili kuongeza tija katika ufugaji.
“Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya mifugo katika uchumi
wa nchi. Ndiyo maana imekuwa ikichukua hatua mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa
majosho, utoaji wa dawa za kuogeshea mifugo pamoja na chanjo ya ugonjwa wa homa
ya mapafu ya ng’ombe (CBPP) kwa gharama nafuu,” alisema Dkt. Choga.
Aliongeza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha ugonjwa huo
unadhibitiwa na hatimaye kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Tunawahakikishia wafugaji kuwa tunaendelea na juhudi za
kutafuta suluhu ya ugonjwa huu, kama tunavyofanya kwa magonjwa mengine ya
mifugo kama homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP), chambavu (Black Quarter) na
kimeta (Anthrax),” alisema.
Katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa huo, wafugaji
wamehimizwa kuzingatia usafi wa mifugo yao, hususan kuogesha mara kwa mara ili
kudhibiti kuenea kwa ugonjwa katika maeneo mengine.



Comments