Na Mwandishi Wetu
Mbeya. Spika wa Bunge Mstaafu, Tulia Ackson, ametoa msaada wa mchele kilo 400 pamoja na Sh4.4 milioni kwa familia 22 zilizoathirika na maafa ya maporomoko ya tope katika Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
Dkt Tulia, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uyole na Rais wa Inter-Parliamentary Union (IPU), alikabidhi msaada huo Aprili 1, 2026 baada ya kutembelea na kukagua maeneo yaliyoathirika kufuatia maporomoko hayo yaliyotokea usiku wa kuamkia Machi 25, 2026, baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.
Katika ziara hiyo, Dkt Tulia alitembelea familia zilizoathirika na kutoa msaada wa chakula pamoja na fedha kwa lengo la kuwafariji wahanga, akisema bado kuna mahitaji makubwa kwa waathirika hao.
“Tumetembelea familia katika kata za Lupepo, Kinyara, Ikuti, Kawetele na Nkunga. Hali siyo nzuri—wengi wamepoteza makazi na wanaishi kwa majirani. Wanahitaji chakula, magodoro na makazi bora. Tunawaomba wadau kujitokeza kusaidia,” amesema.
Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa hatua za haraka zilizochukuliwa tangu kutokea kwa maafa hayo, pamoja na uongozi wa wilaya kwa juhudi za kukabiliana na athari za tukio hilo.
Katika hatua nyingine, Dkt Tulia alitoa wito kwa jamii na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia familia zilizoathirika, akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kipindi hiki kigumu.
Mmoja wa waathirika, Joshua George, mkazi wa kata ya Kinyara aliyepoteza watoto wawili, alimshukuru Dkt Tulia kwa msaada na faraja, akisema hatua hiyo imewapa nguvu ya kuendelea na maisha licha ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rungwe, Mekson Mwakipunga, alisema tukio hilo limeacha majonzi makubwa, huku baadhi ya familia zikibaki bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maporomoko hayo.
Alieleza kuwa katika Kijiji cha Mboyo, familia moja ilipoteza watu wanne, huku mmoja wa wanafamilia akidaiwa kunywa sumu kutokana na maumivu ya kupoteza wajukuu zake watatu.
Mwisho.
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
Comments