Na Friday Simbaya, Iringa
Serikali imeeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Soko la Machinga Complex katika Manispaa ya Iringa, uliopitishwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maeneo rasmi ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, bungeni, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Festo Dugange, alisema mradi huo unatarajiwa kujengwa katika eneo la zamani la stendi ya mabasi, Kata ya Kitanzini, lenye ukubwa wa mita za mraba 6,555 kwa gharama ya Sh bilioni 4.67.
Alifafanua kuwa soko hilo litakuwa na vizimba 800, maduka 150 na migahawa 8, na linatarajiwa kuhudumia wafanyabiashara 958, wakiwemo wafanyabiashara wadogo 800, wa kati 150 pamoja na mama na baba lishe 8.
Kwa mujibu wa Dugange, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetenga Sh milioni 100 kwa ajili ya maandalizi ya awali ya ujenzi wa mradi huo.
Akichangia hoja, Mbunge Ngajilo aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuanzisha mradi huo, akieleza kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Iringa Mjini. Aidha, alihoji kama wafanyabiashara, hususan wamachinga, watahusishwa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo na ni lini utekelezaji utaanza rasmi.
Akijibu hoja hizo, Serikali ilisisitiza kuwa ushirikishwaji wa wadau ni hatua ya msingi katika utekelezaji wa miradi yote ya kimkakati, ikiwemo kuwahusisha viongozi wa halmashauri, madiwani na wafanyabiashara wa eneo husika.
Serikali imeelekeza Manispaa ya Iringa kuandaa andiko la mradi na kuliwasilisha Tamisemi kwa ajili ya tathmini na utafutaji wa fedha za kuunga mkono utekelezaji wake. Pia imesisitiza umuhimu wa halmashauri kuendelea kutenga fedha kila mwaka kupitia mapato ya ndani.
Imeelezwa kuwa baada ya kukamilika kwa hatua za maandalizi, ujenzi wa soko hilo utaanza kwa kuzingatia maoni na mahitaji ya wafanyabiashara waliolengwa kunufaika na mradi huo.

Comments