Baadhi ya majeruhi wa ajali iliyohusisha basi la kampuni ya
Shabiby na lori la mizigo lililokuwa likisafirisha vinywaji baridi aina ya
Pepsi wameeleza kwa masikitiko namna walivyookoka katika tukio hilo lililotokea
katika Kijiji cha Tanangozi, Kata ya Mseke, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Ajali hiyo ilitokea baada ya magari hayo kugongana uso kwa
uso, na kusababisha vifo na majeraha kwa abiria kadhaa.
Mwandishi wa The Guardian alitembelea Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Iringa na kuzungumza na baadhi ya majeruhi wanaoendelea kupatiwa
matibabu, huku wengine wengi wakiwa tayari wameruhusiwa baada ya hali zao
kuimarika.
Mmoja wa majeruhi hao, Juma Shaban, mwalimu wa Songwe Tech
Secondary School mkoani Songwe, alisema wakati ajali inatokea alikuwa amelala
usingizi ndani ya basi akiwa safarini kuelekea Mbeya.
“Nilikuwa nimelala kabisa. Ghafla nikasikia kelele za watu
wakivunja vioo vya basi ili kuwaokoa abiria. Nilipojitambua nilikuwa navuja
damu nyingi na mguu wangu ulikuwa umevunjika,” alisema Juma akiwa wodini.
Majeruhi mwingine, Elias Mwakilomo, mkazi wa Tarime na
mhasibu wa Mgodi wa Nyamongo, alisema alikuwa akisafiri kwenda Mbeya kuhudhuria
msiba wa bibi yake.
“Nilishtuka tu nikijikuta mbavu zangu zimebanwa kwenye siti.
Wananchi wa eneo lile walinisaidia kunitoa, lakini sikuweza kuokoa kitu
chochote,” alisema.
Mwakilomo alisema katika ajali hiyo alipoteza simu yake
pamoja na kompyuta mpakato aina ya MacBook Air. Madaktari walimfanyia upasuaji
mdogo wa kuondoa damu na usaha kwenye kifua, na hali yake inaendelea vizuri.
Naye Ben Lilawola, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI),
ambaye aliumia jicho la kulia, alisema aliona lori likifanya overtake katika
kona kwa mwendo mkubwa kabla ya kuligonga basi walilokuwa wakisafiria.
“Niliona lori likiovertake ghafla. Sekunde chache baadaye
likagonga basi letu. Baada ya hapo nikahisi kitu kizito kimenibana kichwani,”
alisema Ben, ambaye anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa jicho.
Wakati huo huo, ndugu wa raia wa India aliyefariki dunia
katika ajali hiyo wameeleza masikitiko yao kufuatia kifo hicho.
Mmoja wa ndugu hao, Zain Mukadam maarufu kama Kaza Roho,
alisema walifika hospitalini kwa ajili ya kumtambua ndugu yao, Tejas Jaral
(31), lakini baadaye walielezwa kuwa alikuwa amefariki dunia majira ya saa moja
usiku.
Alisema marehemu alikuwa akisafiri kutoka Dodoma kwenda Mbeya
kwa shughuli za kikazi, huku akiishi na kufanya kazi jijini Dar es Salaam.
“Tumeanza mawasiliano na ubalozi kuhusu taratibu za
kusafirisha mwili kwenda India kwa ajili ya mazishi, kwani hapa Tanzania hakuwa
na ndugu wa karibu,” alisema.
Mukadam aliwashauri wasafiri kuhakikisha wanaandika majina
yao sahihi pamoja na namba za simu za ndugu wa karibu ili kurahisisha utambuzi
na mawasiliano wakati wa dharura.
Pia alitoa wito kwa Jeshi la Polisi na kampuni za usafiri
kuhakikisha magari ya abiria yanakuwa na orodha kamili ya wasafiri ili
kurahisisha utambuzi wa waathirika endapo ajali zitatokea.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela, alisema hali za majeruhi wengi zinaendelea vizuri, huku wagonjwa watatu pekee wakiendelea kulazwa hospitalini.
“Kwa sasa wagonjwa watatu wanaendelea kupatiwa matibabu. Hali
zao zinaendelea vizuri na tunawafuatilia kwa karibu,” alisema Dk Mwakalebela.
Ajali hiyo imeacha majonzi makubwa kwa familia za waliopoteza
ndugu zao na kuibua tena mjadala kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama
barabarani ili kuokoa maisha ya Watanzania.
Mwisho
Comments